Rais William Ruto atafanya ziara yake ya kwanza rasmi kama Rais wa tano Pwani wiki hii baada ya kuagiza kwamba huduma za bandari zirejeshwe katika bandari ya Mombasa.

Tamko hilo limepokelewa kwa furaha na washikadau ambao wamemshukuru Dkt Ruto kwa kutimiza ahadi yake ya kampeni kwa kubatilisha agizo lililotolewa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

Uhamisho wa huduma za bandari kutoka Mombasa hadi Bohari ya Kontena ya Nairobi na Naivasha ilikuwa mada kuu katika kampeni za urais katika kaunti za Mombasa na Nakuru.

Viongozi kutoka Mombasa wamekuwa wakiunga mkono kurejea kwa shughuli za bandari katika mji wa pwani, huku wenzao wa Nakuru wakishinikiza uwekezaji zaidi katika ICD ya Naivasha.

Wadau wa bandari wamekaribisha agizo la Dkt Ruto, wakisema hatua hiyo itafufua uchumi.