Familia moja katika kijiji cha Kivuleni eneo bunge la Lungalunga kaunti ya Kwale inamtafuta mwanao wa miaka 17 aliyetoweka kwa muda wa wiki moja sasa baada ya kukosa kujiunga na kidato cha kwanza.

Hii ni baada ya Khalid Idris kupata alama 321 katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE japo alikosa kujiunga na shule ya upili ya Taru aliyokuwa ameitwa kufuatia ukosefu wa fedha.

Hatua hiyo inadaiwa kumchochea Idris kutoroka nyumbani kwa hasira ya kutopelekwa shuleni na wazazi wake wasiojiweza.

Inasemakana kuwa mtoto huyo alikasirishwa na hatua ya wazazi wake ya kushindwa kumpeleka shuleni ili kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari.

Sasa familia hiyo inaitaka serikali kuwasaidia kumpata mtoto wao ili wamtafutie ufadhili wa masomo kutoka kwa wahisani.