Takriban Wakenya 3,000 wamekwama nchini Sudan kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Waziri wa Masuala ya Kigeni na Diaspora Alfred Mutua amefichua hayo huku ripoti zikionyesha kuwa mapigano nchini Sudan yanazidi kuongezeka.

Mutua, hata hivyo, amebainisha kuwa serikali inashughulikia kuwahamisha Wakenya hadi maeneo salama ikiwa hali itazidi kuwa mbaya.

Mapigano yalizuka Jumamosi kuhusu mzozo wa madaraka kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF.

Kamati ya madaktari imeripoti kuwa takriban raia 56 wameuawa huku makumi ya wanajeshi pia wamekufa huku takriban watu 595 wakijeruhiwa.

Majenerali wa Jeshi wamekuwa wakiiongoza Sudan tangu mapinduzi yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa Rais Omar el Bashir Oktoba 2021.