Jamii ya Waboni wanaoishi katika eneo la Mungini kaunti ya Lamu wamelalamikia hali ngumu ya kimaisha kutokana na kukosekana kwa huduma za kimsingi katika eneo hilo.

Wakiongozwa na mzee wa eneo hilo Yusuf Lali wakaazi wao wamesema wanahisi kutengwa na serikali ya kitaifa na hata ile ya kaunti kwani eneo hilo halina shule, kituo cha afya wala barabara na hukubwa na uhaba wa maji kila mara.

Wamesema ukosefu wa shule katika eneo hilo limesababisha vijana wa eneo hilo kukosa elimu jambo ambalo wamesema litazidi kuwatenga na ulimwengu ikizingatiwa kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha hasa katika ulimwengu wa kisasa.

Wamewataka viongozi wa kaunti kushirikiana na wale wa kitaifa kuhakikisha wakaazi hao wanapata huduma za kimsingi za kibinadamu kutoka kwa serikali ili waweze kuishi kama Wakenya wengine katika maeneo mengine ya nchi.