Wakaazi wa ukanda wa Pwani wametahadharishwa dhidi ya kugawanywa kwa mirengo ya kisiasa ,kabila au jinsia na wanasiasa wakati huu taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari hapa Mombasa mwenyekiti wa vuguvugu linalopigania uchumi wa Pwani la Fast Action Business Community Salim Karama amesema ni sharti kwa wakaazi wa Pwani kujitahadharisha na semi za uchochezi hususan katika mitandao ya kijamii.

Karama amesema kwamba semi hizo zinaweza kuwa sababu ya kuzuka kwa ghasia na migawanyiko miongoni mwa jamii zinazoishi katika ukanda huu wa Pwani.

Karama aidha amevitaka vitengo mbalimbali vya kiusalama pamoja na tume ya ushirikiano na utangamano wa kitaifa NCIC na ofisi ya mkuu wa mashtaka kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wanaondeleza siasa za uchochezi nchini.

 Mwandishi:Ibrahim Mudibo