Waziri wa utalii nchini Najib Balala, amesema changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, uwindaji haramu na uharibifu wa mazingira hazijakwamisha juhudi za uhifadhi wa mazingira hapa nchini Kenya.

Akizungumza huko Kasighau kaunti ya Taita Taveta Balala amesema kubuniwa kwa mfumo wa ukusanyaji ushuru kwa njia ya kidijitali kutawezesha taifa hili kukusanya ushuru wa shilingi bilioni saba,kutoka mbuga zote nchini pamoja na kuzuia uhalifu wa mazingira.

Waziri huyo amewapongeza walinda misitu na mazingira huku akiwarai kujizatiti katika kazi yao kwa ujasiri bila uoga, ili kuendeleza uhifadhi wa mazingira na wanyama pori, akiwataka wadau katika sekta hiyo kuwawezesha kikamilifu.

Amewapongeza kutokana na juhudi na umoja wao, akisema juhudi hizo zimewezesha kunaswa kwa pembe karibia kilo 84,000 za ndovu.