Waumini wa Kiislamu jijini Mombasa wameadhimisha swala ya Idd-ul-Fitr katika misikiti mbali mbali huku mvua ikitatiza swala iliyokuwa ifanyike kwa pamoja katika uwanja wa Ronald Ngala.

Kuanzia alfajiri ya siku ya Jumamosi (Aprili 22), matamko ya takbiri ndiyo yaliyohanikiza sehemu mbalimbali za mjini Mombasa na kwingineko wakati Waislamu wakijumuika kwa sala maalum ya Idd-ul-Fitri kusherehekea mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Licha ya hali ya maisha kuwa ngumu kwa ujumla kwa kila mtu, wengi wa waumini waliozungumza na Radio Rahma walisema wanashukuru kwa kuweza "kukidhi gharama za chakula."

Gavana wa kaunti AbdulSwamd Sharif Nassir amewaomba waumini wa dini ya kislam kuendelea na ibada licha ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza baada ya swala ya Eid katika msikiti wa Memon hapa Mombasa amewaomba waumini kuendeleza ibada na kukumbuka jamii maskini.

Aidha gavana Nassir ameliombea amani taifa la Kenya wakati huu ambapo kunashuhudiwa migogoro ya kisiasa.

Naye Waziri wa madini na uchumi wa bahari Salim Mvurya amewataka waumini wa dini ya kiislamu na wakenya kwa jumla kudumisha amani nchini.

Akizungumza wakati wa suala ya kuadhimisha sikukuu ya Idd huko Kwale, Mvurya amewasihi waislamu kuishi kwa umoja na amani baada ya kukamilisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Ni kauli iliyoungwa mkono na mwalimu wa Islamic Tawheed Centre kutoka Maganyakulo Sheikh Shariff Abdallah aliyewataka waislamu wote kuwaheshimu viongozi wao wa kidini.


 

More Stories

Buriani jenerali Francis Ogolla

Idara ya polisi yasema mgomo wa madaktari ni usumbufu

Seneta Miraj amtetea waziri wa afya

Bandari ya Lamu kuipiku ile ya Mombasa asema Mbogo