Wakaazi wa Ndau Lamu Mashariki wameshauriwa kutouza ardhi zao kwa sababu zisizokuwa na msingi pindi watakapopata hatimiliki ya ardhi zao.

Mwakilishi wa wadi ya Kiunga Omar Bwana amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiuza vitu vyao vya thamani kwa sababu ndogondogo kama vile sherehe za harusi.

Amesema kutokana na ahadi ya serikali ya kaunti ya kutaka kutoa hatimiliki za eneo hilo itakuwa vyema watu kutumia aridhi zao kwa njia endelevu badala ya kuziuza kwa bei duni.

Bwana amesema ardhi ni rasilimali inayoweza kutoka kwa kizazi baada ya kizazi hivyo basi haitakuwa jambo la busara kwa mzazi kuuza ardhi kwa kutatua tatizo la muda mfupi.

Aidha amewahimiza wakaazi wa eneo hilo kutumia ardhi zao kwa kilimo hasa kilimo biashara ili kupunguza umaskini na kuboresha maisha yao.