Jumla ya watu Saba wamejitokeza kuwania nyadhfa mbali mbali katika uchaguzi wa muungano wa mabaharia nchini SUK.

Uchaguzi huo unatarajiwa kuandaliwa Juni 24 Mwaka huu katika ukumbi wa Licodep eneo bunge la Likoni.

Kulingana na mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya muungano huo Menza Samson Karisa, maandalizi yote yamekamilika na kwamba uchaguzi utaendelea kama ilivyoratibiwa baada ya mahakama ya leba na ajira kuagiza kuandaliwa uchaguzi upya.

Menza amepuuzilia mbali kundi jengine lililojitokeza na kutangaza uchaguzi mbadala Juni 21 Mwaka huu katika ukumbi wa Mission To Seamen.

Miongoni mwa walioidhinishwa kuwania nyadhfa ni Mwalimu Chii Hamisi na Khalfani Jillani Mwamboje watakaowania nafasi ya mwenyekiti.

David Henry Kibuyu ndiye mwaniaji pekee aliyejitokeza kuwania nafasi ya naibu mwenyekiti.
Wengine ni Apollo Odhiambo Orao na Atie Swaleh Ramadhan watakaomenyana katika nafasi ya katibu mkuu wa muungano huo.

Nafasi ya mweka hazina itawaniwa na John Hussein Zappa na Suleiman Omari Boma.

Ikumbukwe kuwa muungano huo umekumbwa na mzozo wa uongozi ambapo mwezi February Mwaka huu mahakama ya leba ilitoa uamuzi wa kubadilisha uchaguzi ulioandaliwa Mwaka 2021 kwa kukosa kufuata katiba ya muungano huo.

Aidha mahakama hiyo iliagiza muungano huo kuunda bodi ya uchaguzi na kuandaa uchaguzi upya ndani ya siku 90.