Idara ya usalama kaunti ya Mombasa na Pwani kwa jumla imetakiwa kuingilia kati na kuwakamata matapeli wanaodaiwa kuwaibia wakaazi kwa michezo isiyoeleweka.

Matapeli hao wanadaiwa kuendeleza biashara zao katika maeneo ya Feri, Mwembe Tayari na eneo la Mtwapa huko kaunti ya Kilifi kwa kuwaibia wakaazi kupitia kwa simu kwa kuwalaghai.

Kulingana na afisa wa dharura kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la MUHURI Francis Auma, ni kwamba wamepokea kesi Zaidi ya 50 za watu ambao wamelalamikia kulaghaiwa pesa zao na matapeli hao.

Auma aidha amelaumu idara za usalama ile ya kaunti ya Mombasa pamoja na serikali kuu kwa kile anachodai kuwa, licha ya waathiriwa kuripoti visa hivyo hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya matapeli hao huku wakiendelea kuwaibia watu.

Afisa huyo amevitaka vitengo vya usalama kuingilia kati suala hilo na kuwaepusha watu na ulaghai huo.

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na Josphat Maina ambaye alitapeliwa na walaghai hao.

Aidha ameonya kuwa iwapo vitengo vya usalama havitawajibika watalazimika kuchukua hatua mikononi mwao ili kujilinda kutokana na wezi hao.

Walaghai hao wanadaiwa kutokea jijini Nairobi na kuanzisha ulaghai huo kaunti ya Mombasa na Kilifi baada ya ulaghai wao kuangaziwa na runinga moja humu nchini kwa namna walivyokuwa wakiwaibia wakaazi wa mitaa tofauti ya Nairobi.