Mchakato wa kuwania kiti cha ugavana katika kaunti ya Kilifi unaendelea huku wagombea kiti hicho wakionekana kutafuta uungwaji mkono katika kaunti hiyo.

Hatua hiyo inajiri huku tayari wagombea wanne wakiendelea kuunda mikakati ya kisiasa ya kumrithi gavana wa kaunti hiyo Amason Kingi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Naibu waziri wa ugatuzi nchini Gedion Mungaro ambaye ni mmoja wa wagombea wa kiti hicho amepeleka kampeni zake katika eneo la Bamba kaunti ndogo ya Ganze ambapo amewahimiza wananchi kumchagua ili aweze kuleleta maendeleo.

Kulingana na Mungaro,kaunti ya Kilifi itaweza kuzalisha chakula cha kutosha na kuimarisha sekta ya afya pindi tu atakapochaguliwa kuwa gavana wa kaunti hiyo.

Naibu gavana wa kaunti hiyo Gedion Saburi ni miongoni mwa wanasiasa ambao wanataka kumrithi kingi huku akiahidi kuwa yuko na tajriba ya uongozi kwani amekuwa kwenye uongozi wa serikali ya Kilifi.

Spika wa bunge la kaunti hiyo Jimmy Kahindi pia anaendeleza kampeni zake huku akiwaahidi wananchi kuwa atakabiliana na tatizo la uhaba wa chakula na umaskini.

Mbunge wa Malindi Esha Jumwa ameonekana kuendeleza kampeni zake kwa kasi kwa kuwarai wanawake wa kaunti hiyo kushirikiana na kumpigia kura ili aweze kuongoza kaunti hiyo.