Chama cha UDA kaunti ya Kwale kinaendeleza zoezi la kura ya mchujo wa uwakilishi wa wadi pekee baada ya viongozi wanaowania nyadhifa za ugavana, useneta na ubunge kupewa tiketi ya moja kwa moja.

Hata hivyo baadhi ya wanachama wa kaunti hiyo wamelalamikia maandalizi mabovu ya mchujo huo ulioanza kuchelewa katika vituo mbali mbali vya upigaji kura.

Wanachama wameelezea kutoridhishwa kwao na mfumo unaotumika kutambua majina ya wapiga kura katika sajili ya tume ya uchaguzi nchini IEBC

Kwa upande wake mgombea wa kiti cha uwakilishi wa wadi ya Ukunda Ali Mondo aliyepiga kura katika kituo cha Mwakigwena, ameridhishwa na mfumo huo.

Aidha, Mondo ameahidi kushirikiana na wapinzani wake wanaokimezea mate kiti hicho kupitia chama cha UDA endapo atashindwa kwenye mchujo huo.

Wadi zinazoendeleza mchujo huo ni Ukunda, Bongwe Gombato na Mwavumbo.

Wakati huohuo baadhi ya wakaazi wamekitaka chama hicho kufutilia mbali mchujo wa uwakilishi wa wadi ya Ukunda.

Wakaazi hao wanaomuunga mkono mgombea wa kiti cha uwakilishi wa wadi hiyo Gladys Mwakisha wamekitaka chama cha UDA kumpatia tiketi ya moja kwa moja.

Wakiongozwa na Roseline Nafula, wakaazi hao wamesema kuwa Mwakisha anafaa kupewa tiketi hiyo ili kutoa nafasi kwa wanawake zaidi kuwania nyadhifa za kisiasa.

Kwa upande wake mgombea huyo amewataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi ili kumpigia kura katika mchujo wa wadi hiyo.

Mwakisha anatarajiwa kushindana na wapinzani wake Ali Mondo na Hamisi Hatibu wanaokimezea mate kiti hicho kupitia chama cha UDA.

 


 

More Stories

Buriani jenerali Francis Ogolla

Idara ya polisi yasema mgomo wa madaktari ni usumbufu

Seneta Miraj amtetea waziri wa afya

Bandari ya Lamu kuipiku ile ya Mombasa asema Mbogo