Serikali ya Kaunti ya Kilifi, kwa mara nyingine inamulikwa kwa madai ya ufisadi baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuitisha maelezo kuhusu shilingi bilioni 1.1 zinazodaiwa kuwa malipo ya kampuni za uwakili.

Afisa Mkuu wa EACC, Twalib Mubarak, amethibitisha kuwa uchunguzi kuhusu malipo hayo unaendelea.

Baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo wakiongozwa na Seneta Stewart Madzayo, Mbunge wa Kaloleni, Paul Katana, na mwaniaji ugavana (ODM), Gideon Mung’aro walitaka uongozi huo wa Gavana Amason Kingi uzuiwe kulipa pesa zozote hadi uchunguzi utakapokamilika.

Katika miaka iliyopita, EACC ilikuwa imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya sakata za ufisadi katika idara ya afya ya kaunti.

Mung’aro amesema kiasi hicho cha pesa ni kikubwa mno na kinaweza kutumiwa kwa mahitaji mengine muhimu kama vile usambazaji wa maji safi kwa wakazi wa Kilifi.