Huku taifa la Kenya likiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana, serikali pamoja na viongozi mbalimbali wamelaumiwa kwa kutoangazia changamoto zinazowakumba vijana.

Afisa kutoka shirika la kijamii la KECOSCE Mwalimu Rama ameilaumu serikali kuu na zile za kaunti, kwa kutoangazia kwa kina sera za vijana na badala yake vijana wamesalia kutumika visivyo.

Aidha amewanyooshea kidole cha lawama viongozi ambao ni vijana katika nyadhifa tofauti akisema kuwa licha ya wao kuaminiwa na wenzao, wameshimdwa kuyapa masuala ya vijana kipaumbele.

Akizungumza na meza yetu ya habari, afisa huyo aidha amesema kutohusishwa kwa vijana katika mambo tofauti hasa miradi ya maendeleo, ndio imepelekea baadhi yao kutumika na wanasiasa kwa malengo yao binafsi huku wengine wakijiunga na makundi ya kihalifu, akitaka serikali kuwapa kipaumbele vijana katika masuala mbalimbali.

Wakati uo huo, ametaka vijana kujitambua na kujituma katika nyadhifa tofauti za uongozi na kutokubali kutumiwa na wanasiasa wengine kwa maslahi yasiyo ya vijana na kuwa hali hiyo imewaacha vijana wengi wakiumia.