Hatimaye wahudumu wa afya kaunti ya Mombasa wameufutilia mbali mgomo wao uliyokuwa ukiendelea.

Kulingana na mwenyekiti wa muungano wa madktari KMPDU kanda ya Pwani daktari Hassan Ahmad Mkuche wamechukua hatua hiyo kufuatia agizo la mahakama kupitia kesi iliyowasilishwa na serikali ya kaunti ya Mombasa ikitaka kusitishwa kwa mgomo huo.

Aidha Mkuche amesema kuwa japo wameusitisha mgomo huo, bado matakwa yao hayajatimizwa kama walivyokuwa wamepeana kwenye ilani yao kabla ya kuandaa mgomo huo.

Wakati uo huo, daktari Mkuche amesema kuwa huduma za matibabu zitaregelewa kama kawaida katika hospitali zote za umma kaunti ya Mombasa kuanzia kesho Ijumaa, wakisubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa mahakamani kuhusu utata wa mishahara yao pamoja na malipo mengine.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa mnamo Machi 23 mwaka huu.

Mapema wiki jana wahudumu hao wa afya walisusia kazi kutokana na serikali ya kaunti kushindwa kutekeleza matakwa yao ikiwemo kutowalipa mishahara kwa wakati, ambapo kufikia sasa wanadai mishahara ya mwezi Januari na Februari, vilevile kukosa kulipiwa mikopo yao pamoja na malipo mbalimbali ya msingi.

Mwandishi: Ibrahim Juma