Mwenyekiti wa Baraza kuu la ushauri kwa Kiislamu nchini KEMNAC Sheikh Juma Ngao ametilia shaka uongozi wa aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko akisema kwamba Sonko hafai kuwa Gavana wa Kaunti ya Mombasa.

Akizungumza katika Kaunti ya Mombasa hii leo, Sheikh Ngao amemtaja Sonko kama Kiongozi asiyekuwa na maadili na ambaye tayari anakabiliwa na kesi mbalimbali mahakamani zinazofungamana na ufisadi.

Kauli hii inajiri baada ya chama cha WIPER kumuidhinisha gavana huyo wa zamani wa Kaunti ya Nairobi kuwa mgombea wao wa ugavana katika kaunti ya Mombasa

Sheikh Ngao amewasihi Wakaazi wa Kaunti ya Mombasa kujitenga na Sonko na kuwaangazia Viongozi wengine waliyo na maadili na agenda ya maendeleo kwa jamii.

Wakati uo huo, Kiongozi huyo ameshikilia kwamba Viongozi wanaostahili kuongoza jamii ni wale waliyo na sera za kuinua maisha ya jamii na wanaokumbatia amani katika kampeni zao za kisiasa.

 Mwandishi: Ibrahim Juma Mudibo.