Ujumbe wa Marekani umefanya majadiliano na maafisa wa Taliban katika juhudi za kuwezesha kupatikana kwa mabilioni ya dola kutoka kwenye akiba ya benki kuu ya Afghanistan yanayozuiwa nchini Marekani.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema mkutano huo, uliwahusisha mwakilishi maalum wa Marekani anayeshughulikia maswala ya Afghanistan Thomas West, waziri mdogo wa hazina ambaye pia anasimamia maswala ya ugaidi na mienendo ya miamala ya fedha Brian Nelson na maafisa wa Afghanistan walioliwakilisha kundi la Taliban linalotawala nchini Afghanistan.